Tangazo La Nafasi Za Kazi Kutoka Bunge La Jamhuri Ya Muungano Wa Tanzania November 2025

Website Bunge La Jamhuri Ya Muungano Wa Tanzania

Bunge La Jamhuri Ya Muungano Wa Tanzania


JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

OFISI YA BUNGE

TANGAZO LA NAFASI ZA KAZI

Kumb. Na. CEA. 277/324/01A/8
Tarehe: 5 Novemba, 2025


Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeundwa kwa mujibu wa Ibara ya 62 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Aidha, Ibara ya 88 (1) ya Katiba inaunda Sekretarieti ya Bunge yenye jukumu la kuliwezesha Bunge kutekeleza majukumu yake.

Kwa msingi huo, Katibu wa Bunge anatangaza nafasi 28 za kazi katika kada mbalimbali kama ifuatavyo:


1. Mkutubi Daraja la II – Nafasi 2

Majukumu ya Kazi

  1. Kuainisha, kupanga na kuorodhesha machapisho na kusambaza taarifa za Kibunge.
  2. Kutafuta machapisho kulingana na mahitaji ya watumiaji.
  3. Kufanya uhakiki wa mara kwa mara wa machapisho na nyaraka zilizoko maktaba.
  4. Kutoa msaada wa kiufundi kwa Wabunge na Watumishi katika matumizi ya huduma za intaneti na taarifa za kielektroniki.
  5. Kuandaa na kuhifadhi kumbukumbu za watumiaji wa maktaba.
  6. Kutoa mafunzo kwa watumiaji kuhusu mbinu za kutafuta na kupata taarifa.
  7. Kuandaa na kutoa mafunzo ya ndani kwa wasaidizi wa maktaba.
  8. Kusaidia wabunge, watumishi na watumiaji wengine kutafuta taarifa na nyaraka za marejeo.
  9. Kutekeleza majukumu mengine atakayopangiwa na msimamizi wa kazi.

Sifa za Mwombaji

Shahada ya kwanza ya Ukutubi au sifa inayolingana kutoka chuo kinachotambuliwa na Serikali.

Ngazi ya Mshahara: PSS D/1


2. Fundi Sanifu Mfumo wa Maji Daraja la II (Plumber) – Nafasi 2

Majukumu ya Kazi

  1. Kufanya ukaguzi wa kawaida wa mifumo ya maji katika majengo ya Bunge.
  2. Kubuni na kupendekeza mabadiliko madogo ya mifumo ya maji.
  3. Kupendekeza vifaa vinavyohitajika vya mabomba.
  4. Kurekebisha mifumo ya maji na majitaka.
  5. Kufuatilia na kuthibitisha bili za maji.

Sifa za Mwombaji

Cheti cha ufundi (FTC) au Diploma katika Fani ya Mifumo ya Maji kutoka chuo kinachotambuliwa na Serikali.

Ngazi ya Mshahara: PSS C/1


3. Mtakwimu Daraja la II – Nafasi 2

Majukumu ya Kazi

  1. Kuandaa na kushirikisha taarifa za wiki, mwezi na robo mwaka.
  2. Kufanya uchambuzi wa takwimu za fedha, uchumi na bajeti.
  3. Kuandaa takwimu za usimamizi wa vihatarishi na utekelezaji wa bajeti.
  4. Kufanya usuluhishi na uhakiki wa takwimu.
  5. Kuandaa takwimu kwa kuzingatia viwango vya kitaifa na kimataifa.
  6. Kutekeleza majukumu mengine atakayopangiwa.

Sifa za Mwombaji

Shahada ya Takwimu au Hisabati kutoka chuo kinachotambuliwa na Serikali na ujuzi wa kutumia ICT.

Ngazi ya Mshahara: PSS D/1


4. Afisa Ugavi Daraja la II – Nafasi 1

Majukumu ya Kazi

  1. Kutayarisha makisio ya vifaa vinavyohitajika.
  2. Kuandaa utaratibu wa upokeaji na utunzaji wa vifaa.
  3. Kusimamia upokeaji, utunzaji na usambazaji wa vifaa.
  4. Kubuni mfumo wa uwekaji na utunzaji wa vifaa ghalani.
  5. Kuandaa taarifa za vifaa na kutoa taarifa ya thamani ya vifaa ghalani.
  6. Kutayarisha hati za kupokelea vifaa na kusambaza kwa watumiaji.
  7. Kufanya kazi nyingine za fani atakazopangiwa.

Sifa za Mwombaji

Shahada/Stashahada ya Juu ya Ugavi au Professional Level III ya PSPTB na awe amesajiliwa na PSPTB kama “Graduate Procurement and Supplies Professional”.

Ngazi ya Mshahara: PSS D/1


5. Afisa Sheria Daraja la II – Nafasi 3

Majukumu ya Kazi

  1. Kuandaa tafiti za kisheria.
  2. Kutoa ushauri wa kisheria katika chaguzi na mikataba.
  3. Kutoa maoni ya kisheria katika mashauri ya madai na jinai.
  4. Kutoa ushauri katika vikao vya Kamati na Bunge.
  5. Kufanya mawasiliano na ofisi nyingine kwa maelekezo ya maafisa wakuu wa sheria.
  6. Kufanya kazi nyingine atakazopangiwa.

Sifa za Mwombaji

Shahada ya Sheria kutoka chuo kinachotambuliwa na Serikali na awe amehitimu mafunzo ya uwakili yanayotambuliwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Ngazi ya Mshahara: PSS E/1


6. Afisa Habari Daraja la II – Nafasi 3

Majukumu ya Kazi

  1. Kukusanya na kuandika habari.
  2. Kupiga picha mnato na video.
  3. Kuandaa picha za maonyesho, majarida na mabango.
  4. Kutunza picha/maktaba na marejeo.
  5. Kukusanya takwimu mbalimbali zinazohusu habari.
  6. Kufanya kazi nyingine za fani yake atakazopangiwa.

Sifa za Mwombaji

Shahada ya Uandishi wa Habari au Stashahada ya Juu ya Habari kutoka chuo kinachotambuliwa na Serikali, akiwa na ujuzi wa kutumia kompyuta.

Ngazi ya Mshahara: PSS D/1


7. Afisa TEHAMA Daraja la II (System Administrator) – Nafasi 1

Majukumu ya Kazi

  1. Kuchambua mahitaji ya watumiaji wa programu za kompyuta.
  2. Kuandika programu na kufanya majaribio ya programu na mifumo.
  3. Kufanya majaribio ya usanifu wa mifumo ya TEHAMA.
  4. Kufanya majaribio ya user acceptance test.
  5. Kutekeleza majukumu mengine yanayohusiana na TEHAMA.

Sifa za Mwombaji

Shahada au Stashahada ya Juu katika Uhandisi wa Kompyuta, Sayansi ya Kompyuta, Teknolojia ya Habari au Menejimenti ya Mifumo ya Habari.

Ngazi ya Mshahara: PSS E/1


8. Afisa Utafiti Daraja la II – Nafasi 3

Majukumu ya Kazi

  1. Kusaidia kuandaa na kukusanya ripoti za utafiti wa Kibunge.
  2. Kurekodi na kuchanganua takwimu za kazi za utafiti.
  3. Kuhudhuria mikutano ya kanda na kutoa mapendekezo ya tafiti.
  4. Kuandaa ripoti za miradi ya utafiti kwa ajili ya kupitishwa.
  5. Kufanya kazi nyingine za fani yake.

Sifa za Mwombaji

Shahada ya Kilimo, Uchumi wa Kilimo au Uhandisi wa Kilimo kutoka chuo kinachotambuliwa na Serikali.

Ngazi ya Mshahara: PSS D/1


9. Mpokezi Daraja la II – Nafasi 4

Majukumu ya Kazi

  1. Kupokea wageni na kuwasaili shida zao.
  2. Kutunza rejesta ya wageni na simu.
  3. Kuwaelekeza wageni na kupokea simu kutoka ndani na nje.
  4. Kufuatilia ubovu wa vifaa vya mawasiliano.
  5. Kutekeleza kazi nyingine atakazopangiwa.

Sifa za Mwombaji

Astashahada katika Reception, Hospitality, Front Office Operation au Customer Care na ujuzi wa kutumia kompyuta.

Ngazi ya Mshahara: PSS B/1


10. Afisa TEHAMA Daraja la II (Network Administrator) – Nafasi 1

Majukumu ya Kazi

  1. Kusanifu, kusakinisha na kusanidi miundombinu ya ndani na nje ya mtandao wa kompyuta (LAN na WAN).
  2. Kufanya majaribio ya vifaa vya mtandao wa kompyuta.
  3. Kusimamia utekelezaji wa maelekezo ya usalama wa mtandao kwa mujibu wa miongozo ya usalama wa TEHAMA.
  4. Kutathmini na kurekebisha hitilafu za mtandao wa kompyuta.
  5. Kutekeleza kazi nyingine atakazopangiwa na msimamizi wake wa kazi.

Sifa za Mwombaji

Shahada ya Kompyuta katika moja ya fani zifuatazo: Uhandisi wa Kompyuta, Sayansi ya Kompyuta, Elektroniki na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, au mafunzo mengine yanayohusiana na fani hii kutoka chuo kinachotambuliwa na Serikali.

Ngazi ya Mshahara: PSS E/1


11. Mwandishi Taarifa Rasmi za Bunge Daraja la II (Isimu ya Lugha) – Nafasi 1

Majukumu ya Kazi

  1. Kuandika majadiliano ya vikao vya Kamati na Bunge yaliyorekodiwa katika sauti.
  2. Kuandika na kuhakiki michango ya maandishi ya Wabunge.
  3. Kufanya uhariri wa awali wa nakala za majadiliano kabla ya kuziwasilisha kwa Wabunge husika.
  4. Kuingiza masahihisho yaliyofanywa na Wabunge katika nakala za awali za Taarifa Rasmi za Bunge.
  5. Kuhifadhi nakala tepe za awali za majadiliano ya Vikao vya Kamati za Bunge.
  6. Kutekeleza majukumu mengine atakayopangiwa na msimamizi wake wa kazi.

Sifa za Mwombaji

Shahada kutoka Chuo Kikuu au Taasisi ya Elimu ya Juu inayotambuliwa na Serikali katika fani ya Isimu ya Lugha (Linguistics).

Ngazi ya Mshahara: PSS D/1


12. Mwandishi Taarifa Rasmi za Bunge Daraja la II (Uhazili) – Nafasi 2

Majukumu ya Kazi

  1. Kuandika majadiliano ya vikao vya Kamati na Bunge yaliyorekodiwa katika sauti.
  2. Kuandika na kuhakiki michango ya maandishi ya Wabunge.
  3. Kufanya uhariri wa awali wa nakala za majadiliano kabla ya kuziwasilisha kwa Wabunge husika.
  4. Kuingiza masahihisho yaliyofanywa na Wabunge katika nakala za awali za Taarifa Rasmi za Bunge.
  5. Kuhifadhi nakala tepe za awali za majadiliano ya Vikao vya Kamati za Bunge.
  6. Kutekeleza kazi nyingine za kiofisi atakazopangiwa na msimamizi wake wa kazi.

Sifa za Mwombaji

Shahada kutoka chuo kinachotambuliwa na Serikali katika fani ya Utawala na Uhazili (Administration and Secretarial Studies).

Ngazi ya Mshahara: PSS D/1


13. Mhasibu Daraja la II – Nafasi 2

Majukumu ya Kazi

  1. Kuandaa taarifa za mapato na matumizi.
  2. Kuandaa taarifa ya maduhuli na kufanya usuluhisho wa hesabu za benki.
  3. Kupokea maduhuli ya Serikali na kuyaweka benki kwa wakati.
  4. Kukagua hati za malipo.
  5. Kutekeleza majukumu mengine atakazopangiwa na msimamizi wake wa kazi.

Sifa za Mwombaji

Shahada ya Biashara/Sanaa yenye mwelekeo wa Uhasibu au Stashahada ya Juu ya Uhasibu kutoka Taasisi inayotambuliwa na Serikali, pamoja na Cheti cha Taaluma ya Uhasibu CPA (T) au sifa inayolingana inayotambuliwa na NBAA.

Ngazi ya Mshahara: PSS E/1


14. Afisa Usimamizi wa Fedha Daraja la II – Nafasi 1

Majukumu ya Kazi

  1. Kuandikisha na kudhibiti Amana (Securities) za Serikali.
  2. Kufuatilia hati za hisa na maendeleo ya miradi inayofadhiliwa kwa mikopo au misaada.
  3. Kuweka kumbukumbu za madeni ya ndani na nje.
  4. Kusimamia matayarisho ya makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali.
  5. Kufuatilia na kuchambua taarifa za kifedha za kila mwezi (Flash Reports).
  6. Kutekeleza majukumu mengine ya kifedha atakazopangiwa na msimamizi wake wa kazi.

Sifa za Mwombaji

Shahada au Stashahada ya Juu katika fani ya Uchumi na Mipango (Major in Economics), Biashara, Uhasibu au Usimamizi wa Kodi kutoka chuo kinachotambuliwa na Serikali.

Ngazi ya Mshahara: PSS D/1


MASHARTI YA JUMLA

  1. Waombaji wote wawe ni Raia wa Tanzania wenye umri usiozidi miaka 45 (isipokuwa watumishi wa umma).
  2. Waombaji wenye ulemavu wanahamasishwa kutuma maombi na waeleze aina ya ulemavu walionao.
  3. Waambatishe cheti cha kuzaliwa kilichothibitishwa na wakili/mwanasheria.
  4. Watumishi wa umma wapitishe maombi yao kwa waajiri wao husika.
  5. Maombi yaambatane na vyeti vya taaluma vilivyothibitishwa, ikiwa ni pamoja na:
    • Vyeti vya Postgraduate, Degree, Advanced Diploma, Diploma au Certificate.
    • Cheti cha Mtihani wa Kidato cha IV na VI.
    • Cheti cha Kompyuta (Computer Certificate).
    • Vyeti vya kitaaluma kutoka bodi husika.
  6. Vyeti vya matokeo (Testimonial, Provisional Results, Statement of Results) havitakubaliwa.
  7. Waombaji waliosoma nje ya Tanzania wahakikishe vyeti vyao vimehakikiwa na TCU, NECTA au NACTE.
  8. Waliostaafu katika Utumishi wa Umma hawaruhusiwi kuomba isipokuwa kama wana kibali cha Katibu Mkuu Kiongozi.
  9. Uwasilishaji wa taarifa za kughushi haukubaliki na watakaobainika watachukuliwa hatua za kisheria.
  10. Mwisho wa kutuma maombi ni tarehe 18 Novemba, 2025.

JINSI YA KUOMBA

Barua ya maombi ielekezwe kwa:
KATIBU WA BUNGE
Ofisi ya Bunge,
10 Barabara ya Morogoro,
S.L.P. 941,
40490 Tambukareli – DODOMA

Maombi yote yatumwe kupitia mfumo wa Ajira wa kielektroniki (Recruitment Portal):
🔗 https://portal.ajira.go.tz/

Maombi yatakayowasilishwa nje ya mfumo huu hayatapokelewa.


Imetolewa na:
KATIBU WA BUNGE
OFISI YA BUNGE – DODOMA


See also: Why it is Important to always Update your CV to Match the Job Description.

To apply for this job please visit portal.ajira.go.tz.

Spread the love